Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Bodi ya Maji Bonde la Kati

Bodi ya Maji Bonde la Kati

Habari

BODI YA MAJI BONDE LA KATI YAFANYA TATHIMINI YA MAFURIKO YA KARATU


Mnamo tarehe 17/05/2024 Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Kati pamoja na Wataalamu wake wa Mabwawa kwa kushirikiana na wataalamu wa RUWASA Wilaya pamoja na Mhandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu walifika katika eneo lililojaa maji/ Natural depression kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kuanzia tarehe 8 April, 2024.
Maji hayo yanatokea katika milima ya Ngorongoro kupitia Mto Endoro pamoja na maeneo mengine yanayozunguka bonde hilo.Madhara yaliyosababishwa ni pamoja na kuathiri makazi ya watu na nyumba zaidi ya 502 na kaya 800 zimeathiriwa, mashamba, miundo mbinu ya umeme na maji ambapo transfomer moja na visima vitatu vinavyotumiwa na mamlaka ya maji ya karatu yamezamishwa kwenye maji.

Hali ilivyo kwa sasa maji bado yanaendelea kuingia katika bonde hilo hivyo tahadhari ziendelee kuchukuliwa kwa maeneo ambayo bado hayajaathiriwa.

Hatua za muda mfupi zilizopendekezwa ni pamoja na kuchimba utoro wa dharura ili kuyatoa maji yasiendelee kujaa na kuathiri maeneo mengine zaidi.

Hatua za muda mrefu ni kufanya soroveya kwa ajili ya kujua kontua kwa ajili ya kujenga utoro wa maji wa kudumu, kufanya soroveya na usanifu wa kina kwa maeneo ya juu ili kujenga bwawa la kuvuna maji ili yasiweze kuingia kwenye bonde na kama yataingia yawe ni kiasi kidogo na yaingie kwa utaratibu.

Wataalamu wanashauri tahadhari ziendelee kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na madhara ya magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu na magonjwa ya kuhara.

Vyanzo vya maji mbadala vitafutwe kwa ajili ya Wananchi. Tathimini ya madhara yaliyosababishwa na mafuriko ifanyike kwa kina.